MIGOGORO
ya ardhi Tanzania sawa na mgema tembo anayeangushwa na tawi alilozoea kukalia
kila siku wakati wa ugemaji wa pombe hiyo inayotokana na mnazi.
Ebu
fuatilia makala hii ili uweze kupata kujuwa ni nongwa gani inayokwamisha
kupatikana kwa suluhisho la kudumu kuhusu migogoro ya ardhi chini ya kivuli cha
jua la nchi ya Tanzania.
Katika
kudhihirisha hilo, afisa Mifugo mkoa wa Ruvuma Dk. Ramadhani Mwaiganju anaeleza
kwamba, kwa kawaida inapotokea kufanya kazi kwa mazoea bila kuweka mikakati na
njia madhubuti za kudumu kudhibiti migogoro ya ardhi ni sawa kabisa na mgema
tembo anayeangushwa na tawi (kuti) alilozoea kukalia kila siku huku akiamini
kuwa ni imara kumbe limeoza.
Dk.
Mwaiganju anaeleza kwamba, serekali ya
Tanzania pamoja na kwamba migogoro inaibuka siku hadi siku na kumalizwa
kidiplomasia lakini bado suluhisho la kudumu halijatekelezwa ingawa lipo na
linafahamika.
“Serikali
bado haijachukua hatua madhubuti za utatuzi wa migogoro hiyo, kwani ili kuondoa
migogoro ya wakulima na wafugaji lazima serikali ipime ardhi na kutenga maeneo
ya wakulima, wafugaji na wawekezaji ikiwa ni pamoja na kumilikisha ardhi hiyo
kwa vikundi vya wakulima na wafugaji”. Alisema Dk. Mwaiganju.
Unajua
ngoja niwaeleze ndugu zangu, suala la elimu juu ya sheria za ardhi kwa hapa
nchini ni sawa na ule usemi wa wahenga wetu kwamba, “Elimu kwaajili ya wajinga
na Maisha ni kwaajili ya werevu”.
Anaendelea
kueleza afisa huyo wa Ardhi mkoa wa Ruvuma kwamba, kwa mujibu wa sheria ya
ardhi ya mwaka 1999 kifungu namba 5 kimetoa utaratibu wa ugawaji wa ardhi kuanzia ngazi ya kijiji
hadi Mkoa, lakini bado sheria na taratibu hizo zinavyunjwa.
Mfano,
Taasisi ya Uwekezaji Tanzania imepewa nafasi ya kutoa ardhi isiyozidi ekari 500
kwa wawekezaji lakini cha kushangaza wawekezaji wamekuwa wakipewa zaidi ya
hekari 5000 bila kujali maeneno ambayo yanategemewa na wakulima na ufugaji.
Hivyo
ukilichunguza hilo kwa undani utaona kwamba elimu inayotolewa kwa wananchi ili
watoe ardhi kwa waekezaji vijijini au katika hifadhi zilizotengwa kwaajili ya
kilimo ni ile inayoongeza ujinga kwa wananchi na siyo inayolenga kumfanya awe
mwerevu ili afaidi uhuru wake katika kuzitumia na kuzifaidi rasilimali zake.
Ndiyo
maana anaeleza “Tanzania Elimu ni kwaajili ya Wajinga na Maisha ni kwaajili ya
werevu” ambao wanapata ardhi bila kujali maisha ya mifugo ya wananchi katika
eneo husika wala wakulima na matokeo yake migogoro inaibuka kila kukicha.
Anaeleza
suluhisho katika matatizo ya migogoro ya ardhi ni jukumu la serikali kupima na
kutenga ardhi kwaajili ya wakulima, wafugaji na wawekezaji.
Mfano
hai afisa huyo anaeleza kwamba, angalia leo migogoro ya ardhi ikiwemo ile
ya wakulima na wafugaji , Wananchi wa kijiji
cha Ligera wilaya ya Namtumbo Mkoni
Ruvuma, wapo katika mgogoro kati yao na wafugaji wavamizi waliotokea Mbeya na
maeneo mengine ya Morogoro.
Mgogoro
huo, umesababisha pande hizo mbili kuishi katika hali ya wasiwasi bila kujua
hatma ya maisha yao kwani wakati wowote machafuko yanaweza kutokea na hata
kusababisha vifo.
Ama
kweli “majani makavu hayakai karibu na moto”, hivyo ndivyo alivyaanza kueleza katibu
tarafa wa tarafa ya Madaba halmashauri ya Songea aliyefahamika kwa jina la
Dismas Komba. Alieleza
kwamba, tatizo la migogoro ya kimipaka kati
ya wakulima na wafugaji linazidi kuwa kubwa siku hadi siku kwa sababu mkulima
akilima mazao yake, mifugo ya wafugaji lazima ishambulie mazao hayo kwa kula.
Kwa
mantiki hiyo lazima hapo ugomvi na mgogoro mzito utokee lakini endapo mifugo
ingetengewa eneo la mbali la malisho na wafugaji hao basi hilo lisingeweza
kutokea na ndiyo maana nimeanza na kusema ama kweli majani makavu hayakai
karibu na moto na yakikaa lazima yaungue.
Hali
hiyo inatokana na wananchi kujimilikisha ardhi kwa sababu serikali hajawajibika
ipasavyo kayika kuhakikisha inapima na kutenga ardhi kwa ajili ya wakulima na
wawekezaji.
Hivyo
katibu Tarafa huyo anaeleza kwamba jambo la msingi analoliona yeye si vibaya
kama serikali ingechukuwa maamuzi mazito kwanza ya kufuta hati milki
zilizotolewa kwa wawekezaji ili waweke utaratibu upya wa kupima na kutenga
ardhi kwa ajili ya makundi hayo matatu wakuli, wafugaji na wawekezaji.
“Ingekuwa
uamuzi wangu ningefuta hati miliki zote za wawekezaji na za watu wakawaida ili
serikali ipate nafasi ya kujipanga upya kuhusu ugawaji ardhi katika makundi
hayo matatu”. Anaeleza afisa Tarafa.
Hata
hivyo anaeleza kwamba, ni vyema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine
ikazingatia taratibu za uanzishaji vijiji, wilaya na mikoa kwa kuainisha bayana
mipaka ya eneo husika itakayoambatana na kuyatenga maeneo kulingana na makundi
hayo yanayoibua migogoro ya ardhi.
Kijiji
cha Mkindo wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro ni moja ya eneo la mfano wa
migogoro ya ardhi iliyopata kutokea katika nchi hii kati ya wakulima na
wafugaji kama anavyoeleza mmoja wa waathirika wa migogoro hiyo Edina Makubuli.
Migogoro
hiyo imefikia hapo kwa sababu serikali inayo na inajua suluhisho la kudumu la
namna ya kutokomeza tatizo hilo lakini kinachofanyika ni kufanya kazi kwa
mazoea ameeleza makubuli.
Anaeleza
msimamo huo wa serikali wa kufanya kazi kwa mazoea ndiyo unaosababisha migogoro
kutokana na kukosekana kwa utawala bora ambao unapaswa kuangaliwa pia kwenye
suala zima la umilikishaji ardhi kwa mwananchi na wawekezaji.
Viongozi
hao hata kama watapewa taarifa mapema ya kutaka kutokea kwa mapigano kati ya
wakulima na wafugaji, mara nyingi wanapuuzia na kusema hao waongo si jana tu tumetoka
huko na wameelewana huo ni uzushi tu wa watu wachache.
Makubuli
anaeleza matokeo yake jioni utasikia makundi hayo yamechapana, wengine kuuawa
na kujeruhiwa. Hapo ndipo utakapoona viongozi wanajitokeza kwa ajili ya
kuhalalisha posho na si kulipatia suluhisho la kudumu tatizo.
Anaeleza
tatizo hapa linasababishwa na viongozi wa serikali ambao wanapata taarifa
mapema lakini wanachelewa kufika eneo la tukio kwa wakati na matoke yake
yanakuwa mabaya.
Pia
hata wanapofika hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa zaidi ya kulifanya jambo
hilo kana kwamba mgonjwa anayeumwa malaria akapewa dawa aina ya Panaldo ya
kutuliza maumivu na si kupewa dawa ya kutibu ugonjwa husika.
“Kwa
kufanya hivyo mimi kama mmoja kati ya walioathiriwa na migogoro hiyo ninaona
kabisa jambo hili serikali inalifanya kama mradi wao wa kujipatia pesa za
safari kwaajili ya kuelekea kwenye tatizo kwa lengo la kutuliza na si kutibu
tatizo”. Alieleza Makubuli.
Anachoamini
yeye ni kwamba serikali inatumia migogoro ya wakulima na wafugaji kama miradi
bubu ya kuhujumu uchumi wa nchi na kama si hivyo kwanini wasipime na kutenga
maeneo ya makundi hayo? Alihoji Makubuli.
Pia
alihoji hivi ni kiasi gani cha fedha kinatumika kufuatilia migogoro hiyo na kwa
miaka mingapi sasa ambapo bado suala
hilo halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu? Ama kweli Elimu kwaajili ya mjinga na
maisha ni kwaajili ya werevu.
ARDHI
ni rasilmali muhimu sana katika maendeleo ya binadamu, Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake alisema. “ili kupata
maendeleo tunahitaji mambo makuu manne, ardhi, siasa safi, watu,na uongozi
bora”. Kauli hii ilikuwa na lengo la
kuonyesha umuhimu wa ardhi katika suala la maendeleo endapo itatumika na
kusimamiwa ipasavyo.
No comments:
Post a Comment