HAKUNA ubishi kwamba
ardhi ni kitu pekee katika dunia hii ambacho ni cha thamani kufanyia kazi, cha
thamani kugombania kwalo, cha thamani hata mtu
kufa kwa ajii yake, kwasababu ndiyo kitu pekee ambacho kipo daima. Hii
ni tafsiri ya Gerald O’Hara katika riwaya ya toweka na upepo (Gone with the
wind).
Migogoro ya ardhi
Tanzania ni chimbuko la uhasama kati ya wafugaji na wakulima, wafugaji,
wakulima na serikali yao kunakosababishwa na kutokuwepo kwa mipaka, uwekezaji,
kuuzwa na kuuziana kwa viwanja au mashamba ambapo chanzo kikuu cha migogoro hii
ni ukosefu wa elimu ya sheria ya ardhi
kwa watanzania walio wengi.
Fursa inayoonekana
kuwaneemesha waerevu wachache serikalini na miongoni mwa wananchi ambapo ujinga
wao wakutojua sheria za ardhi inakuwa ni mtaji kwa werevu.
Sheria ya Ardhi ya vijiji Na. 5 ya mwaka 1999
ni moja ya sheria ambayo mikakati yake
ni kutekeleza Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995. Sheria hizi zinaainisha
vyombo pekee vya kushughulikia migogoro ya ardhi na nyumba ni Baraza la Ardhi
la kijiji, Baraza la kata, Baraza la Ardhi
na Nyumba la Wilaya, Mahakama Kuu – kitengo cha Ardhi na Mahakama ya Rufaa
Tanzania.
Lakini je, ni kwa kiasi
gani wananchi wanatambua sheria hiyo? kama kunagharama je, wananchi wote
wanaweza kumudu kufungua kesi au mashauri ya migogoro ya ardhi na hata pengine
kuweka wakili? Je, mwananchi wa kawaida katika mazingira haya anaweza kupata
haki yake kiurahisi endapo atapambana na werevu wanaoonekana wanamiliki fedha?
Mimi sina majibu.
Ebu tuangalie mfano hai
wa mgogoro huu wa viwanja kwenye kata ya Mshangano katika Halmashauri ya
Manispaa ya Songea.
Pascal Msigwa ni
mfanyabiashara maarufu mjini Songea ambaye anaeleza kwamba eneo linalodaiwa
kuwa ni la shule ya sekondari si kweli bali ni lake.
“mimi ninalaumiwa bure
lakini kiukweli eneo linalotajwa kuwa ni eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi
wa sekondari ni mali yangu halali kwa kuwa niliuziwa na afisa mmoja wa Idara ya
ardhi Halmashauri ya Manispaa ya Songea.”Alisema Pascal Msigwa.
Alisema eneo hilo
linalodaiwa kuwa lilitengwa kwaajili ya ujenzi wa sekondari Mshangano ni uzushi
na ndiyo maana baada ya kutekeleza taratibu zote za kisheria za ardhi alipewa
eneo hilo.
Kwa upande wake
Mkurugezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Zakaria Nachoo, alipoulizwa
alikana kuhusika katika uuzwaji wa
kiwanja hicho na wala kujua kwamba kuna afisa wake alihusika kutoa eneo hilo
kwa Msigwa.
Ingawa alisema
anaufahamu mgogoro huo ambao kwa hivi sasa upo katika ngazi ya baraza la kata
ambako bado tatizo hilo linashughulikiwa
ili kupatiwa ufumbuzi.
Nachoo alisema elimu
kwa wananchi kuhusiana na sheria ya ardhi ni tatizo kubwa kwasababu katika
mitaa mingi unakuta kwamba pamoja na kuwa viwanja vimepimwa lakini bado
wananchi wanakuwa wakiingia katika migogoro aidha wenyewe kwa wenyewe ama kati
ya wananchi na kampuni ya upimaji.
Akitolea mfano alisema
kwasababu katika mitaa mingi unakuta kwamba pamoja na kuwa viwanja vimepimwa
lakini bado wananchi wanakuwa wakiingia katika migogoro aidha wenyewe kwa
wenyewe ama kati ya wananchi na kampuni ya upimaji.
Alifafanua kwamba mara
nyingi wananchi katika mitaa husika wamekuwa katika migogoro hiyo kutokana na
baadhi ya wenzao kuuza maeneo yasiyowahusu.
Utakuta mtu mwingine
amepakana na mwenzake na yeye anataka kuuza eneo lake, matokeo kwa kuwa mteja
pengine anataka eneo kubwa na kwa fedha nyingi basi mwananchi anauza na eneo ambalo
si lake na kisha kupotea, huo ni ufafanuzi ambao aliutoa Mkurugenzi.
Alisema katika
mazingira haya yameleta mitafaruku mingi kwenye Halmashauri yake ambapo watu
wachache wanatengeneza maisha kutokana na werevu wao huku wakijuwa kwamba
wananchi walio wengi hawana elimu.
Kata ya mshangano
viwanja vyote vilipimwa na kampuni binafsi ijulikanayo kwa jina la “ARDHI PLAN
LIMITED” inayomilikiwa na Samandito Gombo ambaye ni mkurugenzi wa kampuni.
Nachoo alieleza kwamba
kabla ya upimaji maeneo hayo ya Mshangano wananchi walielezwa madhara ya
upimwaji wa viwanja kwa utaratibu wa kampuni hiyo lakini hawakukubali.
Leo migogoro inaibuka
wanakimbilia ofisini kwake kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi jambo ambalo
wananchi hao wangekubaliana na ushauri wao kabla sidhani kama migogoro hiyo
ingefikia hatua iliyopo sasa.
Anaeleza katika moja ya
tukio lililotokea mshangano hivi karibuni, mwananchi alipimiwa kiwanja na kwa
mujibu wa mkataba wa kampuni hiyo ya upimaji wa aridhi, ilikuwa kwa kila mtu mwenye kiwanja kimoja ama viwili
gharama yake ni laki moja kwa kiwanja na laki mbili kwa viwanja viwili.
Kuanzia viwanja vitatu
ilitumika sheria ya uwiano wa 60% kwa 40% ambapo mwanachi angebakiwa na viwanja
sawa na asilimia 60% na kampuni kuchukua asilimia 40% kama malipo ya upimaji wa
viwanja hivyo.
Kwa upande wake afisa
Mtendaji wa mtaa wa Mshangano bwana Damas Mbele amesema kuwa bado wananchi
wanafika ofisini hapo wakiwa na malalamiko kuhusiana na viwanja vyao.
Anaeleza kwamba jambo
hili wanashindwa kulielewa kwa kuwa suala la upimwaji wa viwanja hivyo
lilifanyika kwa maelewano na mikataba ya kisheria kati wananchi hao na kampuni
husika sasa inakuwaje leo wanadai kitu walichotowa kwa hiari yao? Alihoji
mtendaji.
“Inatokea mwananchi
anakuja ofisini akidai kuwa kiwanja ama viwanja
ambavyo kampuni imechukua sivyo
ambavyo yeye alitaka kuipa kampuni na hivyo kufanya migogoro kuendelea
kuwa mingi, kwa kweli jambo hili linatushangaza sana.” Alifafanua Mbele.
Anaeleza kwamba
walipojaribu kufuatilia kwa undani wamegundua kuwa wananchi wameanza kudai tena
viwanja vyao baada ya kuona kwamba wamemaliza fedha ambazo walizipata awali.
Hivyo wanaamini kuwa
kama wataanzisha mgogoro huo basi watapata tena viwanja hivyo kwani kuna baadhi
ya watu wanajifanya mabushi loya ambao wanawachochea wananchi hao ili wadai
tena viwanja.
Huku lengo halisi la
mabushi loya hao ni kutaka kujipatia fedha kutoka kwa wateja wengine kama
endapo maeneo yatapatikana na kuuzwa tena kwa wateja wengine ambao wanakuwa
tayari wamewaandaa.
Alieleza kwamba jambo
lingine ambalo wananchi linawatesa sana ni pale wanapoona afisa ardhi anauza
maeneo ambayo wakati wa kupimwa yalipimwa kwa majina ya watu tofauti lakini
kuuza anauza mtu mmoja.
Alieleza tatizo hili ni
moja ya chanzo cha migogoro kwani hata Halmashauri yao ya Manispaa ya Songea
inachangia kwani hilo jambo la baadhi ya maafisa na madiwani kujigawia maeneo
ni la muda mrefu lakini hakuna suluhisho la kudumu linalochukuliwa.
Pia mbali na hivo
lakini kuna kesi pia za watu kuuza kiwanja kimoja mara mbili ambayo yote pia ni
kutokana na ukosefu wa elimu ya sheria
ya ardhi na nyumba miongoni mwa wananchi wa
Tanzania.
No comments:
Post a Comment