St. Augustine University of Tanzania-Songea

St. Augustine University of Tanzania-Songea
Creating a peaceful society

Thursday, May 21, 2015

Ardhi ya Tanzania inavyowanyonga Watanzania

Na Wanafunzi Mwaka wa Pili, 2015

HAKUNA ubishi kwamba ardhi ni kitu pekee katika dunia hii ambacho ni cha thamani kufanyia kazi, cha thamani kugombania kwalo, cha thamani hata mtu  kufa kwa ajii yake, kwasababu ndiyo kitu pekee ambacho kipo daima. Hii ni tafsiri ya Gerald O’Hara katika riwaya ya toweka na upepo (Gone with the wind).

Migogoro ya ardhi Tanzania ni chimbuko la uhasama kati ya wafugaji na wakulima, wafugaji, wakulima na serikali yao kunakosababishwa na kutokuwepo kwa mipaka, uwekezaji, kuuzwa na kuuziana kwa viwanja au mashamba ambapo chanzo kikuu cha migogoro hii ni ukosefu wa  elimu ya sheria ya ardhi kwa watanzania walio wengi.

Fursa inayoonekana kuwaneemesha waerevu wachache serikalini na miongoni mwa wananchi ambapo ujinga wao wakutojua sheria za ardhi inakuwa ni mtaji kwa werevu.

 Sheria ya Ardhi ya vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 ni moja ya sheria ambayo  mikakati yake ni kutekeleza Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995. Sheria hizi zinaainisha vyombo pekee vya kushughulikia migogoro ya ardhi na nyumba ni Baraza la Ardhi la kijiji, Baraza la kata,  Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Mahakama Kuu – kitengo cha Ardhi na Mahakama ya Rufaa Tanzania.
Lakini je, ni kwa kiasi gani wananchi wanatambua sheria hiyo? kama kunagharama je, wananchi wote wanaweza kumudu kufungua kesi au mashauri ya migogoro ya ardhi na hata pengine kuweka wakili? Je, mwananchi wa kawaida katika mazingira haya anaweza kupata haki yake kiurahisi endapo atapambana na werevu wanaoonekana wanamiliki fedha? Mimi sina majibu.

Ebu tuangalie mfano hai wa mgogoro huu wa viwanja kwenye kata ya Mshangano katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Pascal Msigwa ni mfanyabiashara maarufu mjini Songea ambaye anaeleza kwamba eneo linalodaiwa kuwa ni la shule ya sekondari si kweli bali ni lake.

“mimi ninalaumiwa bure lakini kiukweli eneo linalotajwa kuwa ni eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ni mali yangu halali kwa kuwa niliuziwa na afisa mmoja wa Idara ya ardhi Halmashauri ya Manispaa ya Songea.”Alisema Pascal Msigwa.

Alisema eneo hilo linalodaiwa kuwa lilitengwa kwaajili ya ujenzi wa sekondari Mshangano ni uzushi na ndiyo maana baada ya kutekeleza taratibu zote za kisheria za ardhi alipewa eneo hilo.
Kwa upande wake Mkurugezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Zakaria Nachoo, alipoulizwa alikana kuhusika katika uuzwaji  wa kiwanja hicho na wala kujua kwamba kuna afisa wake alihusika kutoa eneo hilo kwa Msigwa.

Ingawa alisema anaufahamu mgogoro huo ambao kwa hivi sasa upo katika ngazi ya baraza la kata ambako bado tatizo hilo  linashughulikiwa ili kupatiwa ufumbuzi.

Nachoo alisema elimu kwa wananchi kuhusiana na sheria ya ardhi ni tatizo kubwa kwasababu katika mitaa mingi unakuta kwamba pamoja na kuwa viwanja vimepimwa lakini bado wananchi wanakuwa wakiingia katika migogoro aidha wenyewe kwa wenyewe ama kati ya wananchi na kampuni ya upimaji.

Akitolea mfano alisema kwasababu katika mitaa mingi unakuta kwamba pamoja na kuwa viwanja vimepimwa lakini bado wananchi wanakuwa wakiingia katika migogoro aidha wenyewe kwa wenyewe ama kati ya wananchi na kampuni ya upimaji.

Alifafanua kwamba mara nyingi wananchi katika mitaa husika wamekuwa katika migogoro hiyo kutokana na baadhi ya wenzao kuuza maeneo yasiyowahusu.

Utakuta mtu mwingine amepakana na mwenzake na yeye anataka kuuza eneo lake, matokeo kwa kuwa mteja pengine anataka eneo kubwa na kwa fedha nyingi basi mwananchi anauza na eneo ambalo si lake na kisha kupotea, huo ni ufafanuzi ambao aliutoa Mkurugenzi.

Alisema katika mazingira haya yameleta mitafaruku mingi kwenye Halmashauri yake ambapo watu wachache wanatengeneza maisha kutokana na werevu wao huku wakijuwa kwamba wananchi walio wengi hawana elimu.

Kata ya mshangano viwanja vyote vilipimwa na kampuni binafsi ijulikanayo kwa jina la “ARDHI PLAN LIMITED” inayomilikiwa na Samandito Gombo ambaye ni mkurugenzi wa kampuni.

Nachoo alieleza kwamba kabla ya upimaji maeneo hayo ya Mshangano wananchi walielezwa madhara ya upimwaji wa viwanja kwa utaratibu wa kampuni hiyo lakini hawakukubali.

Leo migogoro inaibuka wanakimbilia ofisini kwake kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi jambo ambalo wananchi hao wangekubaliana na ushauri wao kabla sidhani kama migogoro hiyo ingefikia hatua iliyopo sasa.

Anaeleza katika moja ya tukio lililotokea mshangano hivi karibuni, mwananchi alipimiwa kiwanja na kwa mujibu wa mkataba wa kampuni hiyo ya upimaji wa aridhi, ilikuwa  kwa kila mtu mwenye kiwanja kimoja ama viwili gharama yake ni laki moja kwa kiwanja na laki mbili kwa viwanja viwili.
Kuanzia viwanja vitatu ilitumika sheria ya uwiano wa 60% kwa 40% ambapo mwanachi angebakiwa na viwanja sawa na asilimia 60% na kampuni kuchukua asilimia 40% kama malipo ya upimaji wa viwanja hivyo.

Kwa upande wake afisa Mtendaji wa mtaa wa Mshangano bwana Damas Mbele amesema kuwa bado wananchi wanafika ofisini hapo wakiwa na malalamiko kuhusiana na viwanja vyao.

Anaeleza kwamba jambo hili wanashindwa kulielewa kwa kuwa suala la upimwaji wa viwanja hivyo lilifanyika kwa maelewano na mikataba ya kisheria kati wananchi hao na kampuni husika sasa inakuwaje leo wanadai kitu walichotowa kwa hiari yao? Alihoji mtendaji.

“Inatokea mwananchi anakuja ofisini akidai kuwa kiwanja ama viwanja  ambavyo kampuni  imechukua  sivyo  ambavyo yeye alitaka kuipa kampuni na hivyo kufanya migogoro kuendelea kuwa mingi, kwa kweli jambo hili linatushangaza sana.” Alifafanua Mbele.

Anaeleza kwamba walipojaribu kufuatilia kwa undani wamegundua kuwa wananchi wameanza kudai tena viwanja vyao baada ya kuona kwamba wamemaliza fedha ambazo walizipata awali.

Hivyo wanaamini kuwa kama wataanzisha mgogoro huo basi watapata tena viwanja hivyo kwani kuna baadhi ya watu wanajifanya mabushi loya ambao wanawachochea wananchi hao ili wadai tena viwanja.

Huku lengo halisi la mabushi loya hao ni kutaka kujipatia fedha kutoka kwa wateja wengine kama endapo maeneo yatapatikana na kuuzwa tena kwa wateja wengine ambao wanakuwa tayari wamewaandaa.

Alieleza kwamba jambo lingine ambalo wananchi linawatesa sana ni pale wanapoona afisa ardhi anauza maeneo ambayo wakati wa kupimwa yalipimwa kwa majina ya watu tofauti lakini kuuza anauza mtu mmoja.

Alieleza tatizo hili ni moja ya chanzo cha migogoro kwani hata Halmashauri yao ya Manispaa ya Songea inachangia kwani hilo jambo la baadhi ya maafisa na madiwani kujigawia maeneo ni la muda mrefu lakini hakuna suluhisho la kudumu linalochukuliwa.


Pia mbali na hivo lakini kuna kesi pia za watu kuuza kiwanja kimoja mara mbili ambayo yote pia ni kutokana na  ukosefu wa elimu ya sheria ya ardhi na nyumba miongoni mwa wananchi wa Tanzania.  


Migogoro ya Ardhi sawa na Mgema Tembo kuangushwa na Tawi Alilozoea

Na Wanafunzi  wa Mwaka wa Pili 2015


MIGOGORO ya ardhi Tanzania sawa na mgema tembo anayeangushwa na tawi alilozoea kukalia kila siku wakati wa ugemaji wa pombe hiyo inayotokana na mnazi.

Ebu fuatilia makala hii ili uweze kupata kujuwa ni nongwa gani inayokwamisha kupatikana kwa suluhisho la kudumu kuhusu migogoro ya ardhi chini ya kivuli cha jua la nchi ya Tanzania.

Katika kudhihirisha hilo, afisa Mifugo mkoa wa Ruvuma Dk. Ramadhani Mwaiganju anaeleza kwamba, kwa kawaida inapotokea kufanya kazi kwa mazoea bila kuweka mikakati na njia madhubuti za kudumu kudhibiti migogoro ya ardhi ni sawa kabisa na mgema tembo anayeangushwa na tawi (kuti) alilozoea kukalia kila siku huku akiamini kuwa ni imara kumbe limeoza.

Dk. Mwaiganju  anaeleza kwamba, serekali ya Tanzania pamoja na kwamba migogoro inaibuka siku hadi siku na kumalizwa kidiplomasia lakini bado suluhisho la kudumu halijatekelezwa ingawa lipo na linafahamika.

“Serikali bado haijachukua hatua madhubuti za utatuzi wa migogoro hiyo, kwani ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji lazima serikali ipime ardhi na kutenga maeneo ya wakulima, wafugaji na wawekezaji ikiwa ni pamoja na kumilikisha ardhi hiyo kwa vikundi vya wakulima na wafugaji”. Alisema Dk. Mwaiganju.

Unajua ngoja niwaeleze ndugu zangu, suala la elimu juu ya sheria za ardhi kwa hapa nchini ni sawa na ule usemi wa wahenga wetu kwamba, “Elimu kwaajili ya wajinga na Maisha ni kwaajili ya werevu”.

Anaendelea kueleza afisa huyo wa Ardhi mkoa wa Ruvuma kwamba, kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kifungu namba 5 kimetoa utaratibu  wa ugawaji wa ardhi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Mkoa, lakini bado sheria na taratibu hizo zinavyunjwa.

Mfano, Taasisi ya Uwekezaji Tanzania imepewa nafasi ya kutoa ardhi isiyozidi ekari 500 kwa wawekezaji lakini cha kushangaza wawekezaji wamekuwa wakipewa zaidi ya hekari 5000 bila kujali maeneno ambayo yanategemewa na wakulima na ufugaji.

Hivyo ukilichunguza hilo kwa undani utaona kwamba elimu inayotolewa kwa wananchi ili watoe ardhi kwa waekezaji vijijini au katika hifadhi zilizotengwa kwaajili ya kilimo ni ile inayoongeza ujinga kwa wananchi na siyo inayolenga kumfanya awe mwerevu ili afaidi uhuru wake katika kuzitumia na kuzifaidi rasilimali zake.

Ndiyo maana anaeleza “Tanzania Elimu ni kwaajili ya Wajinga na Maisha ni kwaajili ya werevu” ambao wanapata ardhi bila kujali maisha ya mifugo ya wananchi katika eneo husika wala wakulima na matokeo yake migogoro inaibuka kila kukicha.

Anaeleza suluhisho katika matatizo ya migogoro ya ardhi ni jukumu la serikali kupima na kutenga ardhi kwaajili ya wakulima, wafugaji na wawekezaji.

Mfano hai afisa huyo anaeleza kwamba, angalia leo migogoro ya ardhi ikiwemo ile ya  wakulima na wafugaji , Wananchi wa kijiji cha Ligera wilaya ya Namtumbo  Mkoni Ruvuma, wapo katika mgogoro kati yao na wafugaji wavamizi waliotokea Mbeya na maeneo mengine ya  Morogoro.

Mgogoro huo, umesababisha pande hizo mbili kuishi katika hali ya wasiwasi bila kujua hatma ya maisha yao kwani wakati wowote machafuko yanaweza kutokea na hata kusababisha vifo.

Ama kweli “majani makavu hayakai karibu na moto”, hivyo ndivyo alivyaanza kueleza katibu tarafa wa tarafa ya Madaba halmashauri ya Songea aliyefahamika kwa jina la Dismas Komba. Alieleza kwamba, tatizo la migogoro ya  kimipaka kati ya wakulima na wafugaji linazidi kuwa kubwa siku hadi siku kwa sababu mkulima akilima mazao yake, mifugo ya wafugaji lazima ishambulie mazao hayo kwa kula.

Kwa mantiki hiyo lazima hapo ugomvi na mgogoro mzito utokee lakini endapo mifugo ingetengewa eneo la mbali la malisho na wafugaji hao basi hilo lisingeweza kutokea na ndiyo maana nimeanza na kusema ama kweli majani makavu hayakai karibu na moto na yakikaa lazima yaungue.

Hali hiyo inatokana na wananchi kujimilikisha ardhi kwa sababu serikali hajawajibika ipasavyo kayika kuhakikisha inapima na kutenga ardhi kwa ajili ya wakulima na wawekezaji.

Hivyo katibu Tarafa huyo anaeleza kwamba jambo la msingi analoliona yeye si vibaya kama serikali ingechukuwa maamuzi mazito kwanza ya kufuta hati milki zilizotolewa kwa wawekezaji ili waweke utaratibu upya wa kupima na kutenga ardhi kwa ajili ya makundi hayo matatu wakuli, wafugaji na wawekezaji.

“Ingekuwa uamuzi wangu ningefuta hati miliki zote za wawekezaji na za watu wakawaida ili serikali ipate nafasi ya kujipanga upya kuhusu ugawaji ardhi katika makundi hayo matatu”. Anaeleza afisa Tarafa.

Hata hivyo anaeleza kwamba, ni vyema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ikazingatia taratibu za uanzishaji vijiji, wilaya na mikoa kwa kuainisha bayana mipaka ya eneo husika itakayoambatana na kuyatenga maeneo kulingana na makundi hayo yanayoibua migogoro ya ardhi.
Kijiji cha Mkindo wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro ni moja ya eneo la mfano wa migogoro ya ardhi iliyopata kutokea katika nchi hii kati ya wakulima na wafugaji kama anavyoeleza mmoja wa waathirika wa migogoro hiyo Edina Makubuli.

Migogoro hiyo imefikia hapo kwa sababu serikali inayo na inajua suluhisho la kudumu la namna ya kutokomeza tatizo hilo lakini kinachofanyika ni kufanya kazi kwa mazoea ameeleza makubuli.
Anaeleza msimamo huo wa serikali wa kufanya kazi kwa mazoea ndiyo unaosababisha migogoro kutokana na kukosekana kwa utawala bora ambao unapaswa kuangaliwa pia kwenye suala zima la umilikishaji ardhi kwa mwananchi na wawekezaji.

Viongozi hao hata kama watapewa taarifa mapema ya kutaka kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji, mara nyingi wanapuuzia na kusema hao waongo si jana tu tumetoka huko na wameelewana huo ni uzushi tu wa watu wachache.

Makubuli anaeleza matokeo yake jioni utasikia makundi hayo yamechapana, wengine kuuawa na kujeruhiwa. Hapo ndipo utakapoona viongozi wanajitokeza kwa ajili ya kuhalalisha posho na si kulipatia suluhisho la kudumu tatizo.

Anaeleza tatizo hapa linasababishwa na viongozi wa serikali ambao wanapata taarifa mapema lakini wanachelewa kufika eneo la tukio kwa wakati na matoke yake yanakuwa mabaya.

Pia hata wanapofika hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa zaidi ya kulifanya jambo hilo kana kwamba mgonjwa anayeumwa malaria akapewa dawa aina ya Panaldo ya kutuliza maumivu na si kupewa dawa ya kutibu ugonjwa husika.

“Kwa kufanya hivyo mimi kama mmoja kati ya walioathiriwa na migogoro hiyo ninaona kabisa jambo hili serikali inalifanya kama mradi wao wa kujipatia pesa za safari kwaajili ya kuelekea kwenye tatizo kwa lengo la kutuliza na si kutibu tatizo”. Alieleza Makubuli.

Anachoamini yeye ni kwamba serikali inatumia migogoro ya wakulima na wafugaji kama miradi bubu ya kuhujumu uchumi wa nchi na kama si hivyo kwanini wasipime na kutenga maeneo ya makundi hayo? Alihoji Makubuli.

Pia alihoji hivi ni kiasi gani cha fedha kinatumika kufuatilia migogoro hiyo na kwa miaka  mingapi sasa ambapo bado suala hilo halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu? Ama kweli Elimu kwaajili ya mjinga na maisha ni kwaajili ya werevu.


ARDHI ni rasilmali muhimu sana katika maendeleo ya binadamu, Mwalimu Nyerere  enzi za uhai wake alisema. “ili kupata maendeleo tunahitaji mambo makuu manne, ardhi, siasa safi, watu,na uongozi bora”. Kauli hii ilikuwa na lengo la  kuonyesha umuhimu wa ardhi katika suala la maendeleo endapo itatumika na kusimamiwa ipasavyo.

Thursday, April 16, 2015


                                                 


                                                               Peace Journalism Class
                       Thank you the World Family of Radio Maria for Sponsoring the 3 year program

Monday, March 16, 2015

Definition "Peace Theory"

Democratic peace theory is a theory which posits that democracies are hesitant to engage in armed conflict with other identified democracies.

In contrast to theories explaining war engagement, it is a "theory of peace" outlining motives that dissuade state-sponsored violence.